Klabu ya Manchester City ipo hatarini kukumbwa na adhabu nzito ya kupokwa kati ya alama 40 hadi 60 endapo itapatikana na hatia katika kesi ya ukiukaji wa kanuni za kifedha inayomkabili katika Ligi Kuu ya England.
City inakabiliwa na jumla ya mashtaka 115 yanayohusiana na madai ya kukiuka kanuni za kifedha za Premier League, ikiwemo tuhuma za kutotoa taarifa sahihi za mapato na matumizi kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya fedha katika soka la England, iwapo klabu hiyo itapatikana na hatia, adhabu inayoweza kutolewa ni pamoja na kukatwa idadi kubwa ya alama, inayokadiriwa kufikia kati ya 40 na 60. Kiasi hicho cha alama kinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa nafasi ya klabu hiyo kwenye msimamo wa ligi na hata kuiweka kwenye hatari ya kushuka daraja.
Kesi hiyo ilisikilizwa na jopo huru, huku uamuzi wa mwisho ukisubiriwa kutangazwa. Mpaka sasa, hakuna hukumu rasmi iliyotolewa, jambo linaloendelea kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini humo.
Manchester City imeendelea kusisitiza kuwa haina hatia na imekanusha tuhuma zote, ikieleza kuwa ina ushahidi wa kutosha kuthibitisha msimamo wake.
Iwapo adhabu hiyo itatekelezwa, itakuwa miongoni mwa maamuzi makubwa zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya Ligi Kuu ya England, na inaweza kubadili mwelekeo wa ushindani wa msimu husika pamoja na mustakabali wa klabu hiyo yenye mafanikio makubwa katika miaka ya karibuni.