Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza kuongeza kwa kiasi kikubwa fedha za zawadi kwa mashindano yake makubwa ya klabu, CAF Champions League (CAFCL) na CAF Confederation Cup (CAFCC) kuanzia msimu wa 2025/2026.
Tangazo hilo lilitolewa na rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, ambaye alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha ushindani wa soka la klabu barani Afrika na kuongeza mapato ya timu zinazoshiriki mashindano hayo.
Kwa mujibu wa CAF, mshindi wa CAF Champions League sasa atazawadiwa dola za Marekani milioni 6, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 kutoka dola milioni 4 zilizokuwa zikitolewa hapo awali.
Wakati huo huo, mshindi wa CAF Confederation Cup atapata dola milioni 4, kiasi ambacho ni mara mbili ya zawadi iliyokuwa ikitolewa awali ya dola milioni 2.
Katika mgawanyo mpya wa fedha za CAF Champions League, mshindi wa pili atapata dola milioni 2, huku timu zitakazofika nusu fainali zikijipatia dola milioni 1.2 kila moja. Timu zitakazofika robo fainali zitapata dola 900,000, na zile zitakazomaliza nafasi ya tatu au ya nne katika hatua ya makundi zitapata dola 700,000.
Kwa upande wa CAF Confederation Cup, mshindi wa pili atapata dola milioni 1, nusu fainali dola 750,000 kwa kila timu na robo fainali dola 550,000. Timu zitakazomaliza nafasi ya tatu au ya nne katika makundi zitapata dola 400,000.
Aidha, CAF imetangaza kuongeza pia fedha za kusaidia klabu zinazotolewa katika hatua za awali za mashindano hayo kutoka dola 50,000 hadi dola 100,000 ili kusaidia gharama za usafiri na maandalizi ya timu.
Kwa mujibu wa CAF, jumla ya fedha za zawadi katika CAF Champions League sasa imefikia dola milioni 19.6, huku CAF Confederation Cup ikifikia dola milioni 11.9.
Viongozi wa CAF wamesema ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa mapato ya haki za matangazo ya televisheni na mikataba ya udhamini, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani na hadhi ya mashindano ya klabu barani Afrika.
Hatua hiyo inatarajiwa kuzipa motisha klabu mbalimbali barani Afrika kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya CAF.