Prisons yakubali, kukipiga na Yanga Dodoma

Joel JJ By Joel JJ β€’ 11th March 2026


Prisons yakubali, kukipiga na Yanga Dodoma

Afisa Habari wa timu ya Tanzania Prisons Alexander Ngelela amethibitisha mafande hao kuondoka Tabora kuelekea mkoani Dodoma kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga.

Prisons iliwasili Tabora jana tayari kuikabili Yanga kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi hata hivyo Bodi ya ligi imeelekeza mchezo huo kupigwa uwanja wa Jamhuri baada ya dimba la Ali Hassan Mwinyi kukosa sifa.

Ngelela amesema waliiandikia barua Bodi ya ligi juu ya uamuzi wao wa kutumia uwanja wa Ali Hassan Mwinyi baada ya dimba la Sokoine kufungiwa.

"Ni kweli Bodi ya ligi walituandikia barua ya kufungia uwanja wa Sokoine hivyo tukachagua uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kama uwanja wetu wa nyumbani"

"Tuliomba baraka kutoka kwa ndugu Hassan Abdallah ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya ligi, alitoa baraka zote kwamba tunaweza tukaendelea na taratibu nyingine"

"Kwa kuzingatia kanuni za saa 72 ilitulazimu sisi kuanza safari mapema kwa ajili ya kuja hapa Tabora kufanya maandalizi ya mwisho ya mchezo wetu dhidi ya Yanga."

"Tukiwa njiani tulipata barua pepe ambayo ilitutaka tuthibitishe kama tumeruhusiwa kutumia uwanja wa Ali Hassan Mwinyi. Baada ya kuthibitisha, tukaruhusiwa na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kuendelea na taratibu za mchezo"

"Lakini baada ya kufika hapa tukapata barua nyingine kutoka kwa Bodi ya ligi wakitutaarifu kuwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi haujakidhi vigezo. Kwa kuzingatia kanuni ya 17, kifungu cha tano inasema Bodi ya ligi inaweza kuamua vinginevyo na hivyo wameupangia mchezo huu kwenda kuchezwa uwanja wa Jamhuri, Dodoma."

"Sisi kama Tanzania Prisons wajibu wetu ni kufuata taratibu za kikanuni kwa hiyo tunaelekea mkoani Dodoma kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Yanga," alisema Ngelela


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.