Klabu ya Mamelodi Sundowns imeanza vyema hatua ya robo fainali ya mashindano ya CAF Champions League baada ya kuichapa Stade Malien ya Mali kwa mabao 3–0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Ijumaa, Machi 13, 2026 kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld mjini Pretoria.
Sundowns walionyesha ubora mkubwa mbele ya mashabiki wao na kufanikiwa kupata mabao matatu yaliyowapa faida kubwa kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini Mali.
Beki Khuliso Mudau aliifungia Sundowns bao la kwanza dakika ya 34 kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Stade Malien. Kipindi cha pili kilishuhudia wenyeji wakiongeza kasi ya mashambulizi na kufunga bao la pili kupitia mshambuliaji Brayan León Muñiz dakika ya 54.
Shinikizo la Sundowns liliendelea hadi dakika ya 74 pale mshambuliaji Iqraam Rayners alipofunga bao la tatu na kuihakikishia timu yake ushindi mnono wa mabao 3–0.
Ushindi huo unaipa Sundowns nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya nusu fainali kabla ya mchezo wa marudiano utakaoamua mshindi wa jumla ya mabao.
Katika mchezo mwingine wa robo fainali uliochezwa siku hiyo, klabu ya AS FAR Rabat ya Morocco ililazimishwa sare ya bao 1–1 nyumbani na Pyramids FC ya Misri.
AS FAR walipata bao la kuongoza mapema dakika ya nane kupitia kiungo mshambuliaji Ahmed Hammoudan, lakini Pyramids walifanikiwa kusawazisha dakika ya 52 kupitia mshambuliaji Mahmoud Zalaka, matokeo yaliyowaweka wageni katika nafasi nzuri kuelekea mchezo wa marudiano.
Hatua ya robo fainali ya CAF Champions League inaendelea leo kwa michezo mingine miwili mikubwa itakayozikutanisha Esperance ya Tunisia dhidi ya Petro Atlético ya Angola, huku mabingwa wa kihistoria wa mashindano hayo Al Ahly ya Misri wakitarajiwa kumenyana na MC Alger ya Algeria.
Washindi wa jumla ya mabao katika michezo ya robo fainali watafuzu kucheza hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo makubwa ya klabu barani Afrika.