Tetesi za usajili barani Ulaya zinaendelea kushika kasi huku vilabu vikubwa vikianza kupanga mikakati ya kuimarisha vikosi vyao kabla ya dirisha la majira ya joto kufunguliwa. Majina kadhaa makubwa yanaendelea kuhusishwa na mabadiliko ya klabu, huku hatma za baadhi ya nyota zikizua mjadala mkubwa.
Hatma ya Rashford Barcelona Yazua Mjadala
Mshambuliaji wa England, Marcus Rashford (28), anaweza kurejea Manchester United baada ya kipindi chake cha mkopo Barcelona kumalizika mwishoni mwa msimu.
Barcelona inadaiwa kuanza kuangalia mbadala wake, huku winga wa Chelsea na timu ya taifa ya Ureno, Pedro Neto (26), akitajwa kuwa mmoja wa wachezaji wanaofuatiliwa na miamba hiyo ya La Liga.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Rashford mwenyewe angependa kuendelea kubaki Barcelona. Changamoto iliyopo ni mazungumzo kati ya klabu hizo mbili ambayo yanadaiwa kugonga mwamba kuhusu ada ya uhamisho.
Inaelezwa kuwa mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco, amependekeza Rashford aendelee kubaki kwa mkopo kwa msimu mwingine ili kuipa klabu hiyo muda zaidi wa kukusanya fedha za kumununua moja kwa moja kutoka Manchester United.
Tottenham Wapanga Hatma ya Tudor
Tottenham Hotspur wanaendelea kutathmini mustakabali wa benchi lao la ufundi huku wakitazama uwezekano wa kumrithi Igor Tudor iwapo wataamua kufanya mabadiliko ya kiufundi.
Ingawa Tudor anatarajiwa kuendelea kuinoa timu hiyo kwa muda mfupi, ripoti zinaeleza kuwa tayari ameanza kufanya maamuzi magumu kwa kuwatenga baadhi ya wachezaji katika kikosi chake.
Napoli Wataka Kumiliki Hojlund Moja kwa Moja
Napoli wanatarajiwa kuanzisha kifungu cha euro milioni 44 ili kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa Denmark, Rasmus Hojlund (23), ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo kutoka Manchester United.
Iwapo dili hilo litakamilika, Hojlund atakuwa rasmi mchezaji wa Napoli kwa mkataba wa kudumu baada ya kuvutia katika kipindi chake cha mkopo.
Manchester United Watafuta Kocha Mpya
Manchester United wanadaiwa kuwa na orodha fupi ya makocha watano wanaoweza kuchukua nafasi ya Michael Carrick msimu ujao.
Miongoni mwa majina yanayotajwa ni Oliver Glasner wa Crystal Palace, Unai Emery wa Aston Villa, Andoni Iraola wa Bournemouth, kocha wa zamani wa Brighton Roberto De Zerbi pamoja na kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Julian Nagelsmann.
Arsenal Yamvizia Goretzka
Arsenal inaelezwa kujiandaa kuwasilisha ofa rasmi ya kumsajili kiungo wa Bayern Munich na Ujerumani, Leon Goretzka (31), ambaye anatarajiwa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu kama mchezaji huru.
Hata hivyo, Arsenal wanatarajiwa kupata ushindani kutoka AC Milan ambao pia wanavutiwa na huduma za kiungo huyo mwenye uzoefu mkubwa barani Ulaya.
Arsenal Wanaweza Kunufaika na Kiwior
Arsenal wanaweza kupata kiasi cha takriban pauni milioni 1.7 iwapo Juventus wataamua kumsajili beki wa Poland, Jakub Kiwior (26).
Kiwior kwa sasa yupo kwa mkopo katika klabu ya Porto tangu Septemba mwaka jana katika dili lenye kipengele cha kununua kwa takriban pauni milioni 23.
Bastoni Awindwa na Liverpool na Barcelona
Beki wa Inter Milan na Italia, Alessandro Bastoni (26), ameibuka kuwa mmoja wa mabeki wanaotafutwa zaidi katika soko la usajili.
Liverpool wanadaiwa kuonyesha nia ya kumsajili, lakini wanaweza kupata ushindani mkali kutoka Barcelona ambao pia wanatafuta kuimarisha safu yao ya ulinzi.
Tyler Adams Awindwa na Vigogo wa England
Kiungo wa Bournemouth na timu ya taifa ya Marekani, Tyler Adams (27), anatajwa kuwa katika rada za Manchester United ambao wanaongoza mbio za kumsajili.
Hata hivyo, United wanaweza kupata ushindani kutoka Chelsea na Liverpool ambazo pia zimeonyesha kuvutiwa na uwezo wa kiungo huyo.



