Timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', leo Jumapili, Machi 29, 2026, itashuka dimbani kumenyana na Macau katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu wa mashindano ya FIFA Series.
Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Pele uliopo Kigali, ukiwa ni wa mwisho kwa timu zote mbili baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo yao ya awali.
Taifa Stars walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Liechtenstein, huku Macau wakichapwa mabao 4-1 na Aruba, matokeo yaliyowafanya kushindwa kufuzu fainali.
Kutokana na matokeo hayo, Aruba na Liechtenstein wanatarajiwa kukutana katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo ya kirafiki yaliyoandaliwa na FIFA.
Kocha wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, anatarajiwa kufanya mabadiliko ya kikosi chake ili kuimarisha safu ya ushambuliaji ambayo ilionekana kukosa makali katika mchezo uliopita.
Kwa upande wa Macau, nao wanatarajiwa kuingia uwanjani wakisaka ushindi ili kufuta kumbukumbu ya kipigo kizito walichopata dhidi ya Aruba.
Mashindano ya FIFA Series yameanzishwa na FIFA kwa lengo la kuzipa timu mbalimbali nafasi ya kucheza mechi za kirafiki za kimataifa na kuongeza uzoefu wa ushindani.