Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum maarufu kama 'Fei Toto', ameendelea kuwa nguzo muhimu ya timu hiyo baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika misimu mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara.
Msimu wa huu 2025β2026, Fei Toto ameshiriki moja kwa moja katika mabao 11, akifunga mabao sita na kutoa assisti tano. Bao lake dhidi ya Dodoma Jiji mnamo Machi 11, 2026, kwenye ushindi wa 3-0, limemfanya kuvunja rekodi ya mabao ya msimu uliopita aliyokuwa amefunga manne tu.

Msimu wa 2024β2025, Fei Toto aliongoza kwa assisti katika Ligi Kuu Bara baada ya kuisaidia Azam FC kufanikisha mabao 17 (mabao manne na assisti 13). Aidha, mwaka 2024 ulikuwa wa dhahabu kwa nyota huyu, baada ya kuisaidia timu yake kufanikisha mabao 27 (mabao 15 na assisti 12), akimzidi Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyefanikisha mabao 21 (mabao 12 na assisti tisa).
Msimu wa 2023β2024, Fei Toto alifunga mabao 19 ya Ligi Kuu Bara, akishika nafasi ya pili kwa ufungaji miongoni mwa wachezaji, nyuma ya Aziz Ki aliyefunga 21. Pia, alijitokeza katika Kombe la Shirikisho (FA), akiisaidia Azam FC kufika fainali kwenye New Amaan Complex Juni 2, 2024, ambapo walipoteza kwa penalti 6-5 dhidi ya Yanga baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 120.
Kwa misimu mitatu mfululizo, Fei Toto ameonyesha kuwa si tu mchezaji mwenye ubora wa kipekee, bali pia ni kiungo muhimu kinachochochea mafanikio ya Azam FC.