Klabu ya Al Hilal Omdurman imewasilisha rufaa rasmi kwa Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kupinga matokeo ya mchezo wao wa robo fainali ya CAF Champions League dhidi ya RS Berkane, wakidai kuwa wapinzani wao walimchezesha mchezaji asiye na sifa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Al Hilal wanapinga ushiriki wa beki wa Berkane, Hamza El Moussaoui, wakieleza kuwa alikuwa akitumikia adhabu ya kusimamishwa kwa siku 30 kufuatia tuhuma za matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini (doping).
Taarifa za kisheria zinaonyesha kuwa tayari CAF imefungua kesi ya kinidhamu yenye kumbukumbu namba DC23330 dhidi ya mchezaji huyo. Sampuli ya mkojo (Sample A) iliyochukuliwa Januari 24, 2026 ilibainisha uwepo wa kemikali za Prednisone/Prednisolone.
Kwa mujibu wa World Anti-Doping Agency, kemikali hizo zipo katika kundi la S9 (Glucocorticoids) la orodha ya vitu vilivyopigwa marufuku michezoni kwa mwaka 2026.
Aidha, inaelezwa kuwa uamuzi wa awali wa kinidhamu kuhusu suala hilo ulitolewa na CAF Machi 11 mwaka huu, hali inayozua maswali kuhusu uhalali wa mchezaji huyo kushiriki mchezo husika wa robo fainali.
Licha ya RS Berkane kujaribu kupunguza uzito wa tuhuma hizo kwa kueleza kuwa ni taarifa zisizo na msingi, nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa suala hilo lipo katika hatua rasmi za kisheria ndani ya CAF.
Iwapo rufaa ya Al Hilal Omdurman itathibitishwa, hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa dhidi ya Berkane, ikiwemo kupokonywa ushindi au kupewa ushindi wa mezani kwa upande wa Al Hilal.
Hata hivyo, hadi sasa Confederation of African Football haijatoa uamuzi wa mwisho kuhusu shauri hilo, huku mchakato wa kulisikiliza ukiendelea.