Simba kuendeleza ubabe dhidi ya Coastal Union leo?

Joel JJ By Joel JJ β€’ 2nd April 2026


Simba kuendeleza ubabe dhidi ya Coastal Union leo?

Timu ya Simba SC leo Alhamisi, Aprili 2, 2026, itashuka dimbani kuikabili Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 1:00 usiku, unakuja wakati kila timu ikiwa na malengo tofauti, huku Simba wakisaka alama tatu muhimu ili kusogea nafasi ya pili na kuendelea kujiimarisha katika mbio za ubingwa, na Coastal Union wakihitaji ushindi ili kuboresha nafasi yao kwenye msimamo wa ligi.

Simba wanaingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi nzuri dhidi ya wapinzani wao hao wa Tanga, baada ya kushinda mechi nyingi walizokutana katika historia ya hivi karibuni. Takwimu zinaonyesha kuwa katika michezo 23 ya mwisho, Simba wameshinda mara 16, huku Coastal Union wakishinda mara moja pekee, na sare sita.

Aidha, katika michezo 10 iliyopita baina ya timu hizo, Simba hawajapoteza hata mmoja, wakishinda nane na kutoka sare mbili, jambo linalowapa morali kubwa kuelekea pambano la leo.

Kwa upande wa maandalizi, Simba wameonyesha kiwango kizuri katika michezo yao ya karibuni, mchezo wa mwisho wakiifumua TRA United mabao 3-0, ingawa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuruhusu mabao katika baadhi ya michezo yao.

Coastal Union nao wamekuwa wakipambana kurejesha makali yao, huku wakionyesha dalili za kuimarika licha ya kukosa mwendelezo mzuri wa matokeo.

Kocha wa Simba Steve Barker anatarajiwa kuwatumia wachezaji wake tegemeo katika kuhakikisha wanapata ushindi wa nyumbani, huku Coastal Union wakitarajiwa kucheza kwa nidhamu wakitegemea zaidi mashambulizi ya kushtukiza.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku mashabiki wakisubiri kuona iwapo Coastal Union wataweza kuvunja mwiko dhidi ya Simba au kama wekundu hao wa Msimbazi wataendeleza ubabe wao.

Matokeo ya mchezo huo yatakuwa na mchango mkubwa katika msimamo wa ligi, hasa kwa Simba wanaowania nafasi za juu katika mbio za ubingwa wa msimu huu.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.