Klabu ya Simba SC imeendeleza ubabe wake katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa leo Alhamisi, Aprili 2, 2026.
Wekundu wa Msimbazi walimaliza kazi mapema ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, wakipata mabao yao kupitia kwa Suleiman Mwalimu na Ismail Toure, waliotumia vyema nafasi walizopata na kuiweka Simba mbele kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kilishuhudia Simba ikiendelea kutawala mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa za wazi za kufunga mabao zaidi. Hata hivyo, ukosefu wa umakini katika eneo la mwisho uliwanyima nafasi ya kuongeza idadi ya mabao, hali iliyoisaidia Coastal Union kuepuka kichapo kikubwa zaidi.
Mshambuliaji Suleiman Mwalimu alikuwa mmoja wa nyota wa mchezo huo, ingawa anaweza kujilaumu kwa kushindwa kufunga zaidi ya bao moja, kwani alipata nafasi kadhaa ambazo angeweza kuzitumia kufikisha hat-trick. Pamoja na hilo, bao lake limemfanya aendelee kuongoza orodha ya wafungaji ndani ya kikosi cha Simba kwa kufikisha jumla ya mabao sita msimu huu.
Ushindi huo muhimu umeirejesha Simba katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha alama 34, wakiwa nyuma ya vinara wao Yanga SC kwa tofauti ya alama nne pekee. Hata hivyo, Simba bado wana mchezo mmoja wa kiporo, jambo linalowapa matumaini makubwa katika mbio za ubingwa.
Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kuthibitisha uimara wake nyumbani Isamuhyo, huku Coastal Union wakilazimika kurejea kujipanga upya kwa ajili ya michezo ijayo.