Klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam inaripotiwa kuanza mchakato wa kumnasa kiungo mkabaji wa Azam FC raia wa Ghana, James Akaminko, ambaye mkataba wake na klabu hiyo unaelekea ukingoni.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya tasnia ya usajili, Yanga imeanza mazungumzo ya awali ikiwa na lengo la kumsajili kiungo huyo mwenye uzoefu mkubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, katika harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao.
Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kuonyesha nia ya kumsajili Akaminko, ambapo awali klabu hiyo iliwahi kujaribu kumjumuisha katika mazungumzo ya usajili wakati wa mchakato wa uhamisho wa mchezaji Feisal Salum kwenda Azam FC, pamoja na jina la Kipre Junior ambaye kwa sasa anacheza MC Alger ya Algeria.
Kwa kipindi hicho, Azam FC ilifanikiwa kumbakiza kiungo huyo ambaye ameitumikia klabu hiyo kwa misimu minne, akiwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika safu ya kiungo.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hali ya sasa inaweza kuwa tofauti, kutokana na mchezaji huyo mwenyewe kuonyesha nia ya kutafuta changamoto mpya baada ya muda mrefu akiwa Azam FC, jambo linaloweza kufungua milango ya uhamisho wake.
Iwapo Yanga SC itafanikiwa kukamilisha dili hilo, huenda ikawa na mabadiliko katika safu yake ya kiungo, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuachana na Moussa Balla Conte ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo katika klabu ya Raja Casablanca ya Morocco.