Klabu ya Simba SC inaendelea kuimarisha mipango yake ya usajili kuelekea msimu wa 2026/27, huku ikitajwa kuwa kwenye hatua nzuri za kukamilisha dili la winga wa Sekhukhune United ya Afrika Kusini, Keletso Makgalwa.
Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa Simba ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kwa karibu mshambuliaji huyo wa pembeni, ambaye ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji wabunifu zaidi katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga nao wanatajwa kumuwania winga huyo lakini mpaka sasa inaonekana ni Simba iliyopiga hatua kubwa kwenye mchakato wa kumsajili.
Makgalwa anatajwa kuwa pendekezo la kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, ambaye anaendelea na mipango ya kuongeza ubora kwenye eneo la ushambuliaji hasa kwa wachezaji wanaocheza pembeni.
Barker anaamini kasi, ubunifu na uwezo wa mchezaji huyo wa kutengeneza nafasi vinaweza kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi.
Winga mwenye kasi na uwezo wa kutengeneza mabao
Makgalwa, ambaye ni raia wa Afrika Kusini, ni winga anayetumia mguu wa kulia lakini mara nyingi hupendelea kuanzia upande wa kushoto ili kutumia kasi yake, uwezo wa kupiga chenga na kuingia ndani kutengeneza nafasi.
Katika msimu wa 2025/26 akiwa na Sekhukhune United, alionyesha kiwango kizuri akihusika kwenye mabao kadhaa ya timu hiyo. Takwimu zinaonyesha alimaliza msimu akiwa na mchango mkubwa wa kiubunifu, akitoa pasi nyingi za mwisho na kuwa miongoni mwa wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi kwenye kikosi hicho.
Imeelezwa tayari Simba imefikia makubaliano binafsi na mchezaji huyo hatua ya sasa wakiwa kwenye mazungumzo na waajiri wake, Shekhukhune United.
Barker amewekeza kwenye eneo la mawinga falsafa na mbinu zake ikihitaji wachezaji wa aina hiyo katika kutengeneza nafasi.
Simba tayari inafaidika na mawinga wake Anicet Oura na Libasse Gueye ambao wanatengeneza nafasi na kufunga.
Oura na Gueye wamepelekea Barker kumbadilishia majukumu Elie Mpanzu ambaye katika mechi za mwisho wa msimu uliopita, alitumika zaidi kama mshambuliaji wa kati