Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametangaza kufutwa kwa kanuni iliyokuwa ikiziruhusu timu wageni kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa mechi kabla ya siku ya mchezo. Amesema kuanzia sasa utaratibu huo utatumika tu pale timu itakapokuwa inacheza kwenye uwanja husika kwa mara ya kwanza.
Karia amesema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha uendeshaji wa mashindano na kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kutokana na utekelezaji wa kanuni hiyo. Kwa mujibu wake, hakuna sababu ya timu kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja ambao tayari ina ufahamu nao kutokana na kucheza mara kwa mara.
Kanuni hiyo imekuwa chanzo cha migogoro katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, hususani dabi za Simba na Yanga, ambapo kumekuwa na mvutano kuhusu haki ya timu mgeni kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi. Wakati mwingine hali hiyo ilisababisha kuahirishwa kwa michezo na kuzua sintofahamu miongoni mwa wadau wa soka.
Kupitia mabadiliko hayo, TFF inaamini itaondoa mianya ya migogoro isiyo ya lazima kabla ya mechi kubwa na kurahisisha maandalizi ya timu. Hatua hiyo pia inatarajiwa kuongeza utulivu katika uendeshaji wa ligi na kuhakikisha ratiba za mashindano zinaendelea bila usumbufu unaotokana na malalamiko ya kabla ya mchezo.