Mshambuliaji wa kimataifa wa DR Congo, Fiston Mayele, ameanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka baada ya kufikia makubaliano ya kujiunga na klabu ya Al Ahli Tripoli ya Libya akitokea Pyramids FC ya Misri.
Taarifa zinaeleza kuwa kila kitu kuhusu uhamisho huo kimekamilika, huku Mayele akisaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola milioni 5 kwa jumla. Kilichobaki ni kutangazwa rasmi na klabu hiyo ya Libya.
Kutoka Yanga hadi kuwa mmoja wa washambuliaji bora Afrika
Mayele alianza kujizolea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki alipokuwa akiichezea Yanga SC, aliyojiunga nayo mwaka 2021 akitokea AS Vita ya DR Congo.
Akiwa Jangwani, alijidhihirisha kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi, akisaidia Yanga kutwaa mataji ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/23. Mabao yake muhimu dhidi ya timu mbalimbali barani Afrika yalimfanya kuvutia vilabu vikubwa vya bara hilo.
Baada ya mafanikio hayo, Pyramids FC ilimsajili mwaka 2023 kwa dau kubwa, ikiwa ni hatua iliyompeleka kwenye moja ya ligi zenye ushindani mkubwa barani Afrika.
Mafanikio makubwa akiwa Pyramids FC
Akiwa Pyramids, Mayele aliendelea kuthibitisha ubora wake mbele ya lango. Alikuwa miongoni mwa nyota walioiongoza klabu hiyo kutwaa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake, huku akimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
Mbali na ubingwa wa Afrika, alichangia pia mafanikio ya Pyramids katika mashindano mengine ya kimataifa, jambo lililozidi kuinua thamani yake kwenye soko la usajili.
Safari mpya Libya
Baada ya kumaliza mkataba wake na Pyramids FC, Mayele sasa ameamua kujiunga na Al Ahli Tripoli, moja ya klabu zenye historia kubwa nchini Libya.
Inaelezwa kuwa klabu hiyo ilimpa ofa nono iliyomshawishi kuanza changamoto mpya, huku akitarajiwa kuwa miongoni mwa nyota wanaolipwa fdha nyingi na klabu hiyo.