Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeanzisha historia mpya baada ya kutangaza kuwa kwa mara ya kwanza kabisa, wachezaji wa timu itakayotwaa Kombe la Dunia 2026 watazawadiwa pete maalum za ubingwa (Championship Rings), wakifuata utamaduni uliozoeleka katika ligi kubwa za Marekani kama NBA, NFL na MLB.
Kwa mujibu wa mpango huo, pete 30 zitatengenezwa mahsusi kwa ajili ya wachezaji na maafisa wa timu itakayonyanyua Kombe la Dunia, zikiwa kumbukumbu ya mafanikio yao ya kihistoria. Hii ni hatua mpya ambayo FIFA inaamini itaongeza hadhi ya ushindi wa mashindano makubwa zaidi ya soka duniani.
Mbali na pete za mabingwa, FIFA pia itatoa pete 1,996 nyingine kwa ajili ya mashabiki kupitia mauzo rasmi, ili kuwapa nafasi ya kumiliki sehemu ya historia ya Kombe la Dunia 2026 na kusherehekea mafanikio ya timu yao.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa FIFA wa kuboresha uzoefu wa mashindano, kuongeza thamani ya chapa ya Kombe la Dunia na kuwaletea mashabiki bidhaa za kipekee zinazobeba historia ya mchezo.
Iwapo mpango huu utafanikiwa, Kombe la Dunia 2026 litabaki katika vitabu vya historia si kwa ubora wa mashindano pekee, bali pia kwa kuwa toleo la kwanza kuwazawadia mabingwa pete maalum za ubingwa, ishara ambayo imekuwa maarufu kwa mabingwa wa michezo mikubwa nchini Marekani.