Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wameendelea kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu mpya baada ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji chipukizi Hussein Juma Mihambo kutoka Mashujaa FC.
Mihambo, ambaye ana umri wa miaka 19, amesaini mkataba wa miaka minne utakaomuweka Jangwani kwa kipindi kirefu huku akitarajiwa kuwa sehemu ya mradi wa klabu wa kujenga kikosi imara cha sasa na baadaye.
Mshambuliaji huyo anajiunga na Yanga kuongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji, huku akiwa miongoni mwa vipaji vya ndani vinavyopewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika ngazi ya juu ya soka la Tanzania.
Usajili wa Mihambo ni sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanywa na Yanga katika kikosi chake, ikilenga kuongeza ubora na kuhakikisha timu inabaki kuwa na ushindani mkubwa katika mashindano ya ndani na kimataifa.