Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ametangaza rasmi kuwa tamasha la Simba Day 2026 litafanyika Jumamosi, Agosti 8, 2026 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, likiwa ni tukio maalum la utambulisho wa kikosi kitakachoitumikia klabu hiyo katika msimu mpya wa mashindano.
Semaji amebainisha kuwa uamuzi wa kuhamishia tamasha hilo kwenye uwanja wa Uhuru umefanyika ili kupisha matengenezo makubwa yanayoendelea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027)
"Simba Day 2026 itafanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, kutokana na ukubwa wa tamasha hili duniani tunatamani kufanyika kwenye Uwanja wa Mkapa lakini kwa sasa upo kwenye matengenezo hivyo uwanja ambao utatumika ni Uwanja wa Uhuru. Tayari tumefanya ukaguzi na kupokea maelekezo kutoka kwa wasimamizi. Tamasha hilo litatumika pia kuadhimisha miaka 90 ya Simba Sports Club," alisema
Ahmed amesema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri, huku uongozi wa klabu ukiwa umejipanga kuhakikisha mashabiki wanapata burudani pamoja na fursa ya kushuhudia kwa mara ya kwanza wachezaji wapya waliosajiliwa pamoja na nyota watakaobaki kukipigania kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Aidha, Simba Day itakuwa sehemu ya kuhamasisha mshikamano kati ya klabu na mashabiki wake kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho pamoja na mashindano ya kimataifa, huku maelfu ya mashabiki wakitarajiwa kujitokeza kuipa sapoti timu yao.
