Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, klabu ya Yanga SC, wameteka soko la usajili nchini kuelekea msimu wa mashindano wa 2026/27.
Yanga inatajwa kukamilisha rasmi usajili wa kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki, huku wakiendelea kupigana vikumbo kuwania saini za mafowadi Jean Claude Girumugisha na Peter Shalulile.
Harakati hizi za mabosi wa Jangwani zinaashiria nia dhabiti ya kutaka kujenga kikosi tishio kitakachotawala mashindano ya ndani na yale ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAF).
Kurejea kwa Mfalme: Yanga Yavunja Benki kwa Aziz Ki
Baada ya wiki kadhaa za majadiliano, hatimaye Yanga imefanikiwa kumrejesha kundini nyota wao wa zamani, raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki.
Taarifa za uhakika zinasema kuwa klabu hiyo imemwaga kiasi cha dola za Marekani 750,000 (takriban Shilingi bilioni 1.9 za Kitanzania) kwenda kwa klabu ya Al Ittihad Tripoli ya Libya ili kuvunja mkataba wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30.
Aziz Ki, ambaye tayari alikuwa amekamilisha makubaliano binafsi na Wananchi, anaripotiwa kutokuwa na furaha kamili tangu alipotimkia Libya mwezi Januari 2026, jambo lililorahisisha maamuzi yake ya kurejea nchini Tanzania ambako amejenga heshima kubwa.
Vita ya Girumugisha: Al Ahli Tripoli Yaingia Kati na Mabilioni
Wakati dili la Aziz Ki likiwa limekamilika, Yanga inakabiliwa na mtihani mzito katika kumsajili kiungo mshambuliaji wa Al Hilal Omdurman na timu ya taifa ya Burundi, Jean Claude Girumugisha.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21, amekuwa lulu sokoni baada ya kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda msimu uliopita baada ya kun'gara na Al Hilal.
Licha ya wasimamizi wa mchezaji huyo kuvutiwa na ushawishi wa Yanga, miamba ya soka ya Libya, Al Ahli Tripoli, imeingia kwa nguvu ikiripotiwa kuwasilisha ofa ya kufuru ya zaidi ya dola milioni 3 (Shilingi bilioni 7.9).
Inaelezwa uongozi wa Al Hilal tayari umeridhia ofa hiyo ya Waarabu, hali inayowaweka Yanga kwenye mazingira magumu ya kuweza kushinda vita hiyo ya kifedha.
Ushambuliaji Kusukwa Upya: Peter Shalulile atajwa
Kwenye eneo la ushambuliaji wa kati, Yanga inatajwa kuwemo kwenye mazungumzo ya chinichini na fowadi mkongwe wa kimataifa wa Namibia, Peter Shalulile.
Shalulile mwenye umri wa miaka 32, ambaye amemaliza muda wake na miamba ya Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns, anatazamwa kama mtu sahihi wa kuongeza nguvu na uzoefu mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Yanga inapambana kupata saini ya nyota huyo ili kuziba nafasi ya Prince Dube, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona kama uzoefu wake wa michuano mikubwa utatua Jangwani, licha ya kuwepo kwa ushindani kutoka kwa mahasimu wao wa jadi nchini.