Kauli tatanishi zilizotolewa na aliyekuwa kocha wa Mashujaa Fc na timu ya taifa na mdau mkubwa wa soka nchini, Jamhuri Kihwelo 'Julio', zimezua mjadala mzito na kuwagawa wadau wa soka nchini.
Mjadala huo umeshika kasi kufuatia kusambaa kwa vipande vya video katika mitandao ya kijamii, ambapo Julio anaonekana akizungumzia kwa hisia kali mwenendo wa Simba, uhasama wa viongozi, na kile alichokiita "udhalili" unaoikabili klabu hiyo mbele ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC.
Simba Lazima Kuwa Bingwa kwa Njia Yoyote
Katika kauli yake iliyozua taharuki kubwa, Julio alisema Simba haina budi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao kwa "njia yoyote ile", akisisitiza kuwa kuruhusu Yanga kuendelea kutawala soka la nchi itakuwa ni dharau kubwa kwa nembo ya klabu hiyo.
"Kama Simba inataka kuwa bingwa msimu ujao, lazima iwe bingwa kwa njia yoyote ile. Yanga akichukua tena ubingwa, utakuwa ni udhalili mkubwa sana kwetu," alisema Julio katika video hiyo.
Pasua Kichwa Ndani ya Uongozi
Julio hakusita kugusia mgogoro wa chini kwa chini unaofukuta ndani ya uongozi wa Simba. Alidai kuwa hakuna umoja miongoni mwa viongozi waliopo madarakani na wale waliopita, jambo linaloivuruga timu hiyo kiutendaji.
Alimtaja aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', akidai kuwa viongozi hao hawaivani na hawashirikiani kwa dhati kwa maslahi ya klabu.
Alitolea mfano wa mahasimu wao Yanga, akidai kuwa siri ya mafanikio ya timu hiyo ni mshikamano wao
"Yanga hata wakiwa na kikosi kibovu, wakiamua kuwa kitu kimoja wanabeba vikombe. Simba viongozi wetu hawapendani, kila mmoja anamvuta mwenzake chini."
Wadau waishukia, wengine wamuunga mkono
Kauli hizo zimepokelewa kwa hisia tofauti na wadau, wachambuzi, na mashabiki wa soka:
- Wanaompinga: Baadhi ya wadau wamemkosoa Julio wakidai kuwa kauli ya kutaka ubingwa kwa "njia yoyote" inahamasisha michezo michafu nje ya uwanja na inashusha hadhi yake kama mwalimu mwenye leseni kubwa ya soka.
- Wanaomuunga Mkono: Wafuasi wengi wa Simba wamemtetea wakisema ameweka wazi kile kinachowasikitisha mashabiki wengi wa klabu hiyo ambao wamechoshwa na ukata wa mataji na migogoro ya ndani ya uongozi.
Hadi sasa, uongozi wa Simba SC haujatoa kauli rasmi kuhusu aliyosema kocha huyo huku klabu hiyo ikiendelea na mikakati yake ya kusuka kikosi kipya tayari kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.