Mchambuzi wa soka, Salumu Mnolela, amesema hatua ya Yanga SC kutumia mwandishi maarufu wa habari za usajili, Fabrizio Romano, kutambulisha jezi zake mpya za kimataifa za msimu wa 2026/27 si jambo geni katika soka la Tanzania.
Mnolela amesema klabu za Tanzania zimewahi kutumia watu mashuhuri wa kimataifa katika shughuli za utambulisho na uendelezaji wa chapa zao, akitoa mfano wa Simba SC ambayo mwaka 2020 ilihusisha beki wa zamani wa Barcelona na Timu ya Taifa ya Uhispania, Gerard Piqué, katika shughuli iliyohusiana na klabu hiyo.
Amesema matumizi ya majina makubwa ya kimataifa katika masoko na utambulisho wa bidhaa za klabu ni sehemu ya mikakati ya kibiashara inayolenga kuongeza mwonekano na mvuto wa klabu katika soko la kimataifa. Kwa msingi huo, amewataka mashabiki na wadau wa soka kulitazama suala la Yanga kutumia Fabrizio Romano kama sehemu ya ushindani wa kibiashara na ujenzi wa chapa kati ya klabu hiyo na Simba.



