Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu imefuta rasmi adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa mchezaji wa Azam FC, Gibril Sillah, katika mchezo namba 034 dhidi ya Kagera Sugar uliomalizika kwa Azam FC kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kamati kupitia picha jongeo pamoja na taarifa za wataalamu na kujiridhisha kuwa Sillah hakustahili kupewa kadi hiyo. Kamati imesema uamuzi huo umezingatia Kanuni ya 12:8 ya Ligi Kuu inayohusu Usimamizi wa Ligi.
Wakati huo huo, kamati imempa onyo kali mwamuzi wa akiba wa mchezo huo, Greyson Buchard kutoka Kagera, kwa kile ilichokieleza kuwa ni mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 43:1(1.8) inayohusu Udhibiti kwa Waamuzi.



