Yanga SC imeandaa siku maalum ya kumkaribisha mshambuliaji wake Selemani Mwalimu, ambapo mchezo ujao wa timu hiyo umetangazwa kuwa “Sele Day” kwa ajili ya kumpa mapokezi ya kipekee nyota huyo.
Akizungumza kuhusu mpango huo, mmoja wa viongozi na wanachama wa Yanga, Alikamwe, amesema mchezo huo umetengwa maalum kwa ajili ya kumkaribisha Selemani Mwalimu baada ya kujiunga na klabu hiyo.
Amesema siku hiyo itakuwa ya kipekee kwa Wananchi, huku akiwataka mashabiki kushiriki katika maandalizi ya kumpokea mchezaji huyo kwa namna ya pekee.
“Siku ya mchezo huu tumei-Dedicate kwa mchezaji wetu Selemani Mwalimu na itakuwa Sele Day. Ni siku maalumu ya kumkaribisha Selemani Mwalimu Jangwani na kwa kuwa amefanya jambo la kimpira kule Botswana, basi Wananchi tunataka kumkaribisha vizuri.”
Katika kuongeza hamasa kuelekea siku hiyo, Alikamwe pia ametoa wito wa kipekee kwa mashabiki wa Yanga, akiwahimiza kuchagua sehemu moja ya mwili yenye nywele na kuweka bleach, kisha kutuma picha zao kama sehemu ya maandalizi ya “Sele Day.”
Mpango huo unatarajiwa kuongeza shangwe miongoni mwa mashabiki wa Yanga na kufanya siku hiyo kuwa ya kipekee kwa Selemani Mwalimu pamoja na Wananchi watakaofika uwanjani.
Kwa sasa, hamasa imeanza kujengwa kuelekea mchezo huo, huku mashabiki wa Yanga wakisubiri kwa hamu kumpokea rasmi Selemani Mwalimu Jangwani.