Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Doumbia, amekiri kuwa anapitia kipindi kigumu cha kutofunga mabao katika hatua za mwanzo za msimu, akisema hali hiyo ni jambo jipya kwake tangu aanze kucheza soka la ushindani.
Doumbia amesema licha ya kupata nafasi za kucheza, bado hajafanikiwa kufungua akaunti yake ya mabao, hali ambayo amesema haijawahi kumkuta katika hatua kama hii ya msimu.
“Ni mara ya kwanza kabisa kwangu kupitia kipindi cha aina hii, kwa sababu hii ni ligi ambayo ndiyo kwanza imeanza. Kwa hiyo ni jambo la kawaida, hasa unapokuwa unapata nafasi yako ya kwanza. Hivyo, hii ni mara yangu ya kwanza kupitia hali kama hii,” amesema Doumbia.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo anaendelea kupata sapoti kutoka kwa mashabiki wa Simba, huku benchi la ufundi chini ya kocha Steve Barker likionyesha imani kwake licha ya changamoto hiyo ya kufunga.
Doumbia pia ameendelea kuonyesha dalili za uwezo wake kila anapopewa nafasi. Katika dakika chache alizocheza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mighty Wanderers, mshambuliaji huyo alionyesha ubora na uwezo wa kuleta tofauti katika safu ya ushambuliaji.
Kwa sasa, kinachosubiriwa ni Doumbia kupata bao lake la kwanza, ambalo linaweza kuwa mwanzo wa kuondoa presha na kumfungulia njia ya kurejea kwenye kiwango ambacho mashabiki wa Simba wanakitarajia kutoka kwake.