Mustakabali wa Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Papy Kimoto, ndani ya kikosi hicho unadaiwa kuwa shakani, huku kukiwa na ripoti kuwa uongozi wa klabu hiyo unafikiria kumfuta kazi kufuatia kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma leo.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, mbali na matokeo hayo mabaya ya uwanjani, hakuna maelewano mazuri kati ya kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mabosi wake.
Chanzo cha kuaminika kimebainisha kuwa mgogoro huo ulisababishwa na hitaji la Kocha Kimoto kutaka wachezaji wote waliosafiri kwenda Sudan Kusini kwa ajili ya michuano ya CAF kuelekea moja kwa moja Kigoma.
Hata hivyo, uongozi ulikataa mpango huo kwa sababu za kiuchumi na kiwepesi, na badala yake ukaagiza wachezaji 12 pekee wasafiri kwa ndege kuungana na kikosi kilichokuwa kimebaki Singida, jambo ambalo linatajwa kumkasirisha kocha huyo.