Simba imeendelea kuweka rekodi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL) ikiting raundi ya kwanza kibabe kwa ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Mighty Wonderers ya Malawi.
Ndio Mnyama ameweka kambani mabao sita katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Uhuru na hivyo kusonga mbele hatua ya awali kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1.
Simba ilitawala mchezo huo tangu mapema tu na vijana wa kocha Steve Barker walihitaji dakika 8 kufunga bao la kwanza lililowekwa kambani na Clatous Chama baada ya kupasiana na nicet Oura.
Ulikuwa mchezo wa upande mmoja ambapo hadi mapumziko Simba ilikuwa mbele kwa mabao 3-1 Chama akiweka kambani mabao mawili na moja likifungwa na Libasse Gueye.
Libasse akaongeza bao la nne mapema kipindi cha pili kabla ya Keletso Makgalwa aliyeingia kuchukua nafasi ya Anicet Oura kuweka kambani bao la tano dakika ya 87 na Morice Abraham kupigilia msumari wa mwisho dakika za lala salama.
Zilikuwa dakika 90 bora kwa vijana wa Simba, wakituma salamu kwenye michuano hii kuwa msimu huu wana dhamira kubwa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa.