Mashabiki wa Simba wameendelea kuonyesha imani kwa mshambuliaji wao Ibrahim Doumbia, wakiamini kuwa ni suala la muda tu kabla ya nyota huyo kutoka Mali kuanza kufungua akaunti yake ya mabao katika mechi za mashindano.
Jana, Doumbia alikuwa sehemu ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kilichoibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Mighty Wanderers katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Ushindi huo uliifanya Simba kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1, baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza.
Licha ya Simba kufunga mabao mengi katika mchezo huo, Wanamsimbazi bado wanasubiri kwa hamu kushangilia bao la kwanza la Doumbia katika mechi za mashindano. Mshambuliaji huyo alipewa nafasi kadhaa dhidi ya Mighty Wanderers, lakini hakufanikiwa kuzitumia na kuweka mpira wavuni.
Hata hivyo, hali hiyo haijawafanya mashabiki wa Simba kumpotezea imani. Badala yake, wameendelea kumuunga mkono wakiamini kuwa uwezo alionao utamwezesha kuanza kufunga pindi atakapopata utulivu na kujiamini zaidi mbele ya lango.
Ni suala la muda tu
Baadhi ya mashabiki wamesema kutokufunga kwa Doumbia katika michezo yake ya mwanzo si sababu ya kuanza kumuweka kwenye presha. Wanaamini mshambuliaji huyo ataendelea kupata nafasi na hatimaye kufungua akaunti yake ya mabao.
Doumbia pia anaonekana kuendelea kufurahia sapoti anayopata kutoka kwa mashabiki wa Simba, hali ambayo inampa nafasi ya kucheza bila kubeba presha kubwa kutoka nje ya uwanja.
Mgunda naye atoa matumaini
Katika mchezo huo dhidi ya Mighty Wanderers, kocha Steve Barker alimpa nafasi pia mshambuliaji Ismail Mgunda, ambaye alisajiliwa kuimarisha safu ya ushambuliaji kufuatia kuondoka kwa Suleiman Mwalimu aliyejiunga na Yanga siku moja kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Mgunda alicheza kwa muda mfupi, lakini alionyesha kiwango kilichowapa matumaini mashabiki wa Simba kwamba anaweza kuwa chaguo muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Uwepo wa Doumbia na Mgunda unaongeza ushindani ndani ya kikosi, huku kila mmoja akitakiwa kutumia nafasi atakazopata kuhakikisha anaisaidia Simba kupata matokeo.