London Metropolitan Police wameandaa operesheni kubwa ya kiusalama katika maeneo ya South East London kuelekea mchezo wa derby kati ya Millwall na West Ham, utakaochezwa kesho. Polisi wameweka dispersal order katika maeneo mbalimbali huku wakijiandaa kudhibiti usalama kabla, wakati na baada ya mchezo huo.
Takribani maafisa 400 wa polisi watatumwa kwenye maeneo mbalimbali kuzunguka mchezo huo, huku operesheni hiyo ikihusisha pia vikosi vya mbwa, polisi waliopanda farasi pamoja na matumizi ya kamera za utambuzi wa sura zinazofanya kazi moja kwa moja (live facial recognition). Kwa mujibu wa Standard Sport, hatua hizo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuhakikisha usalama unadhibitiwa siku ya mchezo.
Mchezo huu una umuhimu wa kipekee kutokana na historia ya ushindani kati ya Millwall na West Ham, ambayo imefikia miaka 126. Derby hii maarufu ya London imekuwa na historia ndefu ya ushindani, huku kurejea kwa mchezo huo kukitarajiwa kuvuta hisia kubwa kutoka kwa mashabiki wa pande zote mbili.
Zaidi ya hapo, mchezo wa kesho utakuwa Dockers Derby ya kwanza baada ya miaka 14, jambo linaloongeza hamu na msisimko kuelekea pambano hilo. Kwa kuzingatia historia ya timu hizo na muda mrefu tangu zikabiliane katika derby hii, mchezo huo unatarajiwa kuwa na presha kubwa ndani na nje ya uwanja.
MILLWALL VS WEST HAM — DOCKERS DERBY
Mchezo utapigwa kesho, huku mashabiki wakisubiri kuona sura mpya ya moja ya derby zenye historia ndefu katika soka la London.