Klabu ya Simba imepanga kuweka kambi ya muda mfupi nchini Afrika Kusini kuanzia Septemba 24, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ratiba yenye ushindani mkubwa ikiwemo Kariakoo Derby, mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ali, amesema kikosi hicho kitaelekea Afrika Kusini mara baada ya kurejea kwa wachezaji ambao hawana majukumu na timu za taifa.
Kwa mujibu wa Ahmed, uongozi umeamua kutumia siku 10 za kambi hiyo badala ya kuendelea na maandalizi ya kawaida katika eneo la Bunju, Dar es Salaam, kwa lengo la kuipa timu mazingira tulivu zaidi ya kufanya maandalizi kuelekea ratiba ngumu ya mwezi Oktoba.
“Kambi hii imesimamiwa moja kwa moja na Rais wa heshima Mohamed Dewji ‘Mo’, ambaye ameona siku hizi 10 badala ya kuendelea kufanya mazoezi Bunju, timu iweke kambi ya muda mfupi Afrika Kusini kwa ajili ya utulivu na kufanya maandalizi yetu,” alisema Ahmed.
Aliongeza kuwa mwezi Oktoba utakuwa na ratiba yenye michezo mbalimbali kwa Simba, hivyo kambi hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya timu kabla ya kuanza kwa majukumu hayo.
“Mwezi wa 10 utakuwa wa ‘moto’ kutokana na ratiba ya michuano mbalimbali ambayo Simba inashiriki, hivyo kambi hii imezingatia mahitaji yetu kuelekea ratiba hiyo ngumu,” alisema.
Kambi hiyo haitawahusisha wachezaji ambao wameitwa katika majukumu ya timu za taifa. Simba ina jumla ya wachezaji saba walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, ambao ni Nathaniel Chilambo, Vedastus Masinde, Bakari Msimu, Nickson Kibabage, Anthony Mligo, Yusuph Kagoma na Moricce Abraham.
Nickson Kibabage ameitwa akiwa bado anauguza jeraha, huku wachezaji wengine wakitarajiwa kuwa na majukumu ya kimataifa katika kipindi hicho.