Mshambuliaji wa DR Congo, Andy Bobwa Boyeli, ameibukia nchini Zambia baada ya kujiunga rasmi na klabu ya Power Dynamos, inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia.
Boyeli amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu na mabingwa hao wa ligi kuu ya Zambia, akianza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka baada ya kuachana na klabu ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini.
Mshambuliaji huyo mwenye asili ya DR Congo amejiunga na Power Dynamos akiwa mchezaji huru, baada ya kumaliza mkataba wake na Sekhukhune United.
Boyeli si mgeni katika soka la Afrika Mashariki, baada ya kuwahi kuvaa jezi ya Young Africans (Yanga SC) ya Tanzania, kabla ya kuendelea na safari yake ya soka katika ligi ya Afrika Kusini.
Aliitumikia Yanga msimu uliopita kwa mkopo ambao hata hivyo ulisitishwa baada ya miezi sita tu baada ya Wananchi kutoridhishwa na kiwango chake.
Amerejea tena Power Dynamos klabu iliyomtambulisha awali na kumpa nafasi ya kusajiliwa na Sekhukhune United.