Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo Alhamisi, Septemba 24, 2026, itakutana na Sudan katika mchezo wa fainali ya mashindano ya kufuzu AFCON U-20 kwa ukanda wa CECAFA, unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Uhuru kuanzia saa 9:30 alasiri, huku Tanzania ikiingia fainali ikiwa haijaruhusu bao katika michezo yake mitatu ya mashindano. Ngorongoro Heroes ilianza kwa kuifunga Rwanda 3-0, Ethiopia 4-0 na Burundi 2-0 katika nusu fainali.
Kwa upande wa Sudan, imefika fainali baada ya kuichapa Uganda mabao 3-2 katika nusu fainali, huku ushindi huo ukiifanya timu hiyo kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia yake kucheza AFCON U-20.
Tanzania na Sudan tayari zimekata tiketi ya kushiriki AFCON U-20 Ghana 2027 baada ya kufika fainali, huku mchezo wa leo ukibaki kuamua bingwa wa ukanda wa CECAFA. Ngorongoro Heroes, ambayo ni mabingwa watetezi baada ya kutwaa taji hilo mwaka 2024, itakuwa ikisaka kulihifadhi kombe hilo mbele ya mashabiki wa nyumbani.