Waziri mwenye dhamana ya Michezo, Paul Makonda, amesema suala la fedha halijawa kikwazo katika maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya AFCON 2027, akieleza kuwa ujenzi na maboresho ya viwanja yanaendelea vizuri.
Makonda amesema Uwanja wa Arusha umefikia asilimia 90 ya utekelezaji, huku Uwanja wa Fumba, Zanzibar, ukiwa umefikia asilimia 85, pamoja na vifaa vya ujenzi kuwa tayari katika eneo la mradi.
Akizungumzia Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Makonda amesema unaendelea kufanyiwa maboresho makubwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kufanyiwa mabadiliko katika eneo la VIP na kuongezwa kwa skyboxes.
βUwanja wa Arusha ni asilimia 90, Benjamin Mkapa kuna mabadiliko makubwa, tumefumua VIP na tunaongeza skyboxes, Fumba ni asilimia 85 na vifaa vipo site,β amesema Makonda.
Makonda pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za kutekeleza miradi hiyo zinapatikana, akisisitiza kuwa hadi sasa maandalizi ya miundombinu ya AFCON 2027 hayajakwama kutokana na suala la fedha.
Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda, huku maboresho ya miundombinu yakiwa sehemu muhimu ya maandalizi ya michuano hiyo.