Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema uongozi wa FC Barcelona umeahidi kuwaleta nchini Tanzania wachezaji wa klabu hiyo iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu.
Makonda ameyasema hayo Septemba 24, 2026, akielezea ziara yake ya siku nne nchini Hispania na mazungumzo aliyofanya na uongozi pamoja na wachezaji wa Barcelona. Ziara hiyo ilihusisha pia mazungumzo kuhusu ushirikiano katika maendeleo ya soka, ikiwemo ukuzaji wa vipaji na mafunzo ya kiufundi.
Katika ziara hiyo, Makonda alikutana na baadhi ya nyota wa Barcelona, akiwemo Lamine Yamal, Pedri, Raphinha na Gavi, huku akiwakaribisha kutembelea Tanzania.
Ahadi hiyo imekuja wakati Tanzania ikiendelea kujiandaa kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda, huku Serikali ikitafuta fursa za kutumia mahusiano na taasisi kubwa za soka duniani katika kukuza vipaji na kuimarisha maendeleo ya soka nchini.