Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Scaloni, amethibitisha rasmi Cristian “Cuti” Romero kuwa nahodha mpya wa Albiceleste, akichukua nafasi ya Lionel Messi ambaye amestaafu kuitumikia timu hiyo kimataifa.
Scaloni amesema Romero tayari alikuwa nahodha wa tatu nyuma ya Messi na Nicolás Otamendi, hivyo ameamua kumpa beki huyo jukumu la kuongoza Argentina katika kipindi kipya baada ya kuondoka kwa Messi. “Nahodha atakuwa Cuti. Tayari alikuwa wa tatu baada ya Leo na Ota,” alisema Scaloni.
Romero amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Argentina katika miaka ya hivi karibuni, akiwa sehemu ya timu iliyotwaa Copa America, Finalissima na Kombe la Dunia la 2022. Scaloni pia ametaja Emiliano Martínez, Rodrigo De Paul na Lautaro Martínez kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuvaa kitambaa cha unahodha endapo mazingira yatahitaji.
Uteuzi wa Romero unakuja wakati Messi akielekea kucheza mechi yake ya mwisho kwa Argentina dhidi ya Benin, Oktoba 6, 2026, katika Uwanja wa Monumental jijini Buenos Aires. AFA imethibitisha mchezo huo kuwa sehemu ya kumuaga Messi baada ya zaidi ya miaka 20 ya kuitumikia timu ya taifa.