Familia ya aliyekuwa mwanachama na shabiki maarufu wa Yanga SC, Haji Omari Ramadhani Mpili, imetoa shukrani kwa Rais wa klabu hiyo kwa namna alivyomhudumia marehemu wakati wa kipindi cha ugonjwa wake hadi alipofariki dunia. Shukrani hizo zilitolewa na mwanaye wakati wa msiba wa Mzee Mpili uliofanyika Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.
Mzee Mpili alifariki dunia usiku wa Jumapili, Septemba 27, 2026, katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri alipokuwa akipatiwa matibabu. Mazishi yake yalifanyika Jumatatu, Septemba 28, katika Makaburi ya Msikiti Mkuu, Ikwiriri.
Katika msiba huo, viongozi mbalimbali wa Yanga walifika kutoa heshima za mwisho, akiwemo Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Alexander Ngai, Ofisa Mtendaji Mkuu Andre Mtine na Meneja wa Habari Ally Kamwe. Mamia ya wananchi pamoja na mashabiki wa Yanga, Simba na Azam pia walishiriki katika mazishi hayo.
Akizungumza baada ya mazishi, Ngai alisema Mzee Mpili alikuwa mwanachama aliyekuwa akiipigania Yanga kwa muda wote wa maisha yake. Klabu hiyo pia ilitoa ubani wa Sh1.1 milioni, huku kundi la wanachama wa Black Card likikabidhi Sh3 milioni kwa familia ya marehemu.