Mlezi wa Simba Queens, Fatema Dewji, ameendelea kuonyesha dhamira yake katika kuendeleza soka la wanawake nchini Tanzania baada ya kuizawadia timu hiyo Sh milioni 20 pamoja na televisheni ya LG kufuatia ushindi wa Ngao ya Jamii ya Wanawake dhidi ya JKT Queens.
Simba Queens ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga JKT Queens 1-0, huku zawadi hiyo iliyotolewa kwa kushirikiana na MeTL Group ikiwa sehemu ya kutambua mchango wa wachezaji, benchi la ufundi na kila aliyeshiriki katika mafanikio ya timu.
Katika mashindano hayo pekee, zaidi ya Sh milioni 40 zimetumika katika kuisaidia na kuizawadia Simba Queens.
Tangu Fatema Dewji alipokuwa Mlezi wa Simba Queens mwaka 2021, timu hiyo imeendelea kujenga rekodi ya mafanikio ndani na nje ya Tanzania.
Simba Queens imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania mara nne, ukiwemo wa msimu wa 2025/26 ambapo ilimaliza na pointi 57.
Hatua nyingine kubwa ilikuja mwaka 2022, Simba Queens ilipotwaa ubingwa wa CECAFA na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake baada ya kushinda mechi zote tano za kufuzu, ikifunga mabao 18 na kuruhusu bao moja pekee.
Baadaye, timu hiyo iliiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake nchini Morocco, ambapo katika ushiriki wake wa kwanza ilifika hatua ya nusu fainali na kumaliza nafasi ya nne barani Afrika.
Kwa Fatema Dewji, mafanikio ya Simba Queens yanaenda sambamba na dhamira pana ya kuwapa wanawake nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kuhakikisha soka la wanawake linapata hadhi, uwekezaji na sapoti inayostahili.
Pia amewataka mashabiki wa soka nchini kuvuka mipaka ya ushabiki wa klabu na kujitokeza viwanjani kuziunga mkono timu za wanawake.