Rais wa Shirikisho la Soka la Ureno (FPF), Pedro Proença, ametoa kauli kali ya kumuunga mkono Cristiano Ronaldo kufuatia sintofahamu iliyozuka kati ya nyota huyo na kocha wa timu ya taifa, Jorge Jesus.
Proença amemtaja Ronaldo kama mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya soka, akisisitiza kuwa ameitumikia Ureno kwa zaidi ya miongo miwili na amekuwa sehemu kubwa ya utambulisho wa taifa hilo. Kwa mujibu wake, mchango wa Ronaldo kwa soka la Ureno hauwezi kupuuzwa.
Akizungumzia mvutano uliotokea kati ya Ronaldo na Jorge Jesus, Proença amesema suala hilo linapaswa kuchukuliwa kama kutokuelewana kati ya mchezaji na kocha, na kwamba halipaswi kugeuzwa kuwa mgogoro wa muda mrefu. Amesema mazungumzo ya aina hiyo ni sehemu ya kawaida ya maisha ya timu na yanapaswa kutatuliwa ndani ya kikosi.
Proença pia amesisitiza kuwa Ronaldo bado anastahili kuwa sehemu ya timu ya taifa kwa kuzingatia ubora wake wa kisoka, huku akisema milango ya timu ya taifa iko wazi kwake endapo atakuwa fiti na kocha atamhitaji. Kauli hiyo inaendana na msimamo wa Jorge Jesus, ambaye pia amesema Ronaldo anaweza kurejea iwapo ataamua kufanya hivyo.
Ronaldo aliondoka kwenye kambi ya Portugal baada ya kutocheza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Norway, licha ya kufanyiwa mazoezi ya kujiandaa kuingia uwanjani, huku baadaye akisema aliamua kuondoka kambini baada ya mazungumzo na Proença. Tangu hapo, kumekuwa na maswali kuhusu mustakabali wake ndani ya timu ya taifa.
Hata hivyo, kwa sasa ujumbe kutoka kwa viongozi wa soka la Ureno unaonekana kuwa wazi: Ronaldo bado ni sehemu ya mipango ya Portugal. Proença amesema baada ya kukamilika kwa mechi nne za awali kuna muda na utulivu wa kukaa pamoja na kutafuta suluhisho la kutokuelewana huko.
Ronaldo, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Portugal akiwa na mabao 146 katika mechi 234 za kimataifa, sasa anaweza kuwa na nafasi ya kurejea kikosini katika dirisha lijalo la kimataifa ikiwa ataamua kuendelea kuitumikia nchi yake.