Cristiano Ronaldo amevunja ukimya na kueleza kwa kina kilichotokea kati yake na kocha wa timu ya taifa ya Portugal, Jorge Jesus, akisema ameamua kueleza ukweli huo yeye mwenyewe baada ya kuahidi kuwa atatoa maelezo ya kile kilichotokea katika kambi ya mwisho ya timu hiyo.
Ronaldo amesema tangu kabla ya Kombe la Dunia 2026 alikuwa tayari ameandaa barua ambayo angeitumia kuwaaga rasmi wananchi wa Portugal baada ya kumaliza safari yake na timu ya taifa. Hata hivyo, baada ya mashindano hayo, rais wa Shirikisho la Soka la Portugal (FPF), Pedro Proença, alimsihi abadili uamuzi huo kwa sababu shirikisho lilitaka aendelee kuitumikia timu ya taifa.
Ronaldo amesema Proença pia alimshirikisha kuhusu uchaguzi wa kocha mpya wa Portugal, huku akimpa nafasi ya kutoa maoni yake. Ronaldo alidai alimpendekeza Jorge Jesus kuwa chaguo sahihi, na ndiyo maana alifurahia Jesus alipoteuliwa. Baadaye Jesus aliwasiliana naye na kumweleza kuwa anamhitaji katika mradi wake mpya, akisisitiza kwamba uwepo wa Ronaldo ulikuwa muhimu kwa timu.
Kwa mujibu wa Ronaldo, katika mazungumzo yao ya awali Jesus alimweleza mpango wa matumizi yake, ambapo angeanza mchezo wa kwanza na wa mwisho wa kambi, huku akipumzishwa katika baadhi ya michezo kwa ajili ya usimamizi wa mwili. Jesus pia alipendekeza Ronaldo asisafiri na timu kwenda Norway na Denmark, lakini Ronaldo alikataa kwa sababu aliona isingekuwa mfano mzuri kwa nahodha wa timu ya taifa kubaki nchini wakati wenzake wakisafiri. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Simão Coutinho, mkurugenzi wa michezo wa Al Nassr.
Ronaldo amesema kabla ya kambi kuanza, Jesus alimtembelea nyumbani kwake Lisbon na mazungumzo yao yalikwenda vizuri huku makubaliano ya awali yakiendelea kuwa vilevile. Ronaldo alianza mchezo dhidi ya Poland huko Alvalade na alipobadilishwa hakulalamika, hata yeye mwenyewe akimkabidhi Bruno Fernandes kitambaa cha unahodha. Hata hivyo, mambo yalibadilika siku ya mchezo dhidi ya Norway, ambapo msaidizi wa Jesus alimfuata wakati wa chakula cha mchana na kumweleza kuwa kocha alitaka kuzungumza naye.
Ronaldo amesema alishangaa baada ya Jesus kumuuliza kama alikuwa fiti kucheza dakika 30, licha ya mpango wao wa awali kwamba angecheza mchezo uliofuata dhidi ya Denmark huko Dragão. Ronaldo alikubali ombi hilo na akaambiwa awe tayari kwa ajili ya kuingia uwanjani. Alianza kupasha misuli moto tangu kipindi cha pili, lakini dakika ziliendelea kwenda bila kuitwa kuingia. Kwa mtazamo wa Ronaldo, hapo ndipo makubaliano yao yalipovunjwa. Tukio hilo likawa chanzo kikubwa cha sintofahamu kati yake na Jesus na hatimaye Ronaldo akaondoka kwenye kambi ya Portugal.