Pamba Jiji FC imezinduka kwa kishindo kikubwa katika Ligi Kuu ya NBC baada ya kuishindilia Geita Gold mabao 4-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ushindi huo wa kwanza msimu huu umepatikana kwa kishindo huku safu ya ushambuliaji ikionyesha makali ya kipekee tangu dakika ya kwanza ya mchezo huo.
Wenyeji Pamba Jiji walionyesha nia ya kusaka alama tatu mapema ambapo mshambuliaji Mafie alifungua karamu ya mabao kwa goli la mapema, kabla ya Diomande kuongeza bao la pili lililoifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ileile ambapo safu ya ulinzi ya Geita Gold ilijikuta ikipoteza umakini na kuruhusu Mayombya kupachika bao la tatu, kisha Msabila akagonga msumari wa mwisho wa nne na kuhitimisha kipigo hicho kizito kwa wageni.
Ushindi huu muhimu unampa nafasi ya kupumua kocha mkuu, Francis Baraza, ambaye alitumia vyema mapumziko ya kalenda ya FIFA kusuka upya makosa ya kikosi chake.
Kwa upande wa Geita Gold, kipigo hiki kinawaacha wakijipanga upya kurekebisha safu yao ya ulinzi ambayo ilionekana kuzidiwa kasi na kukubali kupokea "4G" hiyo ya mshangao jijini Mwanza