Msemaji wa Simba SC, Ahmed Ally, amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani na kufurahia mchezo bila kuwa na presha, akisisitiza kuwa soka ni sehemu ya burudani na furaha kwa mashabiki.
Ahmed amesema siku ya mchezo inapaswa kuwa siku ya kufurahia timu yao, kuwapa moyo wachezaji na kuonyesha upendo kwa klabu, badala ya kuingia uwanjani wakiwa na hofu au shinikizo kubwa la matokeo.
Akizungumzia uteuzi wa Ibrahim Doumbia kuwa mgeni rasmi, Ahmed amesema uamuzi huo umetokana na safari ngumu aliyopitia mchezaji huyo kabla ya kufikia hatua aliyonayo sasa.
Ameeleza kuwa Doumbia amekumbana na changamoto mbalimbali, lakini mashabiki hawakupaswa kukata tamaa juu yake.
Ahmed ameongeza kuwa Doumbia alikuwa mchezaji wa mwisho kuingia uwanjani, lakini kitendo chake cha kuingia kiliibua hisia kubwa kwa mashabiki, ambao walisimama na kumpigia makofi kama ishara ya kumtambua na kumtia moyo.
Aidha, Ahmed amesisitiza kuwa wachezaji hutofautiana katika muda wanaohitaji ili kuzoea mazingira ya timu na kuanza kufanya vizuri.
Ametolea mfano Nathaniel Chilambo, ambaye alianza kuonyesha kiwango kizuri mapema, huku Doumbia akihitaji muda zaidi kuzoea.
Amesema ni muhimu mashabiki kuwa na subira na kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wote wa Simba SC.