Msemaji wa Simba SC, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 de Agosto utachezwa Jumapili, Oktoba 25, 2026, saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Uhuru.
Ahmed amesisitiza muda wa kuanza kwa mchezo huo, akiwakumbusha mashabiki kuwa mchezo uliopita ulianza saa 9:00 alasiri.
Ahmed amesema kikosi cha Simba kimerejea salama nchini Tanzania kikitokea Equatorial Guinea, kilikokwenda kucheza mchezo wa ugenini. Ameongeza kuwa maandalizi ya mchezo wa Jumapili, ndani na nje ya uwanja, tayari yameanza.
Aidha, Ahmed ametangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni Shilingi 5,000 kwa viti vya Mzunguko, Shilingi 30,000 kwa VIP na Shilingi 150,000 kwa Platinum.
Amesema tiketi zote zitauzwa kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa klabu kwenye tovuti ya https://simbasc.wanaut.com. Ahmed ameeleza kuwa klabu imeufanyia tathmini mfumo huo wa mauzo ya tiketi na kuridhika kuwa utafanya kazi vizuri.
Amewataka mashabiki wa Simba kukubali mabadiliko ya kiteknolojia, akisisitiza kuwa klabu inapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia ili kurahisisha huduma kwa mashabiki wake.
“Tunasisitiza na kuwakumbusha Wanasimba kwamba dunia imebadilika, na sisi Simba Sports Club ni watu wa mwaka wa mbele, hivyo lazima twende na mabadiliko ya teknolojia.
Mara nyingi tunafanya mauzo ya tiketi siku ya mwisho kwa sababu baadhi ya watu wanaona tabu kwenda vituoni kununua tiketi. Sasa ukiwa kazini, nyumbani au kwenye daladala, unaweza kununua tiketi yako kwa njia ya mtandao,” alisema Ahmed Ally.