Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Young Africans (Yanga SC), wameendeleza ubabe wao baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Wananchi walionyesha kandanda la kuvutia, wakitawala mchezo kwa kasi na presha kubwa iliyowafanya Kagera Sugar kupata wakati mgumu kujenga mashambulizi kutoka eneo lao la nyuma.
Yanga walianza kwa kasi wakitafuta bao la mapema, na Peter Shalulile alifanikiwa kuuweka mpira wavuni, lakini bao hilo lilikataliwa na mfumo wa mapitio ya video (FVS) kutokana na kuotea.
Hata hivyo, dakika ya 26 Shalulile aliandika bao halali baada ya kumalizia vizuri krosi ya Maxi Nzengeli na kuipatia Yanga uongozi wa 1-0.
Dakika sita baadaye, Wananchi waliongeza bao la pili kupitia Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', aliyemalizia pasi maridadi ya Stephane Aziz Ki na kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Yanga iliendelea kuonyesha ubora wake huku Ibrahim Toure akiingia kama mchezaji wa akiba na kuibadilisha zaidi hali ya mchezo.
Toure alifunga bao la tatu dakika ya 87 kwa kichwa akimalizia krosi ya Zimbwe Jr, kabla ya kukamilisha shoo yake kwa kufunga bao la nneakimalizia krosi ya Clement Mzize.
Ushindi huo wa mabao 4-0 umeipa Yanga nguvu mpya katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC, ukiirejesha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.