Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imebaini dosari za kifedha na kiufundi katika miradi ya ukarabati wa viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru jijini Dar es Salaam, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Arusha, vinavyoandaliwa kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Dosari hizo zimewasilishwa bungeni jijini Dodoma Novemba 3, 2026, na Mjumbe wa Kamati hiyo, Beng'i Issa, ambaye ameeleza kasoro mbalimbali zilizobainika baada ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika ukaguzi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Kamati imebaini kutofungwa kwa mashine nne za udhibiti wa umeme (switchgear), mapungufu katika udhibiti wa ubora wa kazi zilizotekelezwa, pamoja na malipo ya kazi ambazo hazikufanyika na baadhi ya kazi zilizolipiwa zaidi ya thamani yake halisi.
Mbali na Mkapa, PAC imebaini pia changamoto katika miradi ya Uwanja wa Uhuru na Uwanja wa Arusha, ikiwemo matumizi ya vifaa vyenye ubora usioridhisha, uteuzi wa wazabuni wenye bei za juu pamoja na kasoro za kiusanifu zilizosababisha gharama za miradi kuongezeka tofauti na makadirio ya awali.
Kutokana na hali hiyo, Kamati imeitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu dosari zilizobainika, kuhakikisha fedha zilizolipwa kinyume na utaratibu zinarejeshwa na wahusika kuwajibishwa, sambamba na kuchukua hatua za kurekebisha kasoro za kiufundi zilizojitokeza katika miradi hiyo.