Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba SC, Elie Mpanzu, ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba 2026 wa Ligi Kuu ya NBC, huku kocha Steven Barker wa Simba akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) Novemba 5, 2026, Mpanzu alitwaa tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika michezo mitatu iliyochezwa ndani ya mwezi Oktoba na kupata kura nyingi za mashabiki.
Mpanzu aliwashinda washindani wake Iddi Selemani wa Azam FC na Nathaniel Chilambo wa Simba, ambao pia walikuwa wameingia fainali ya tuzo hiyo. Katika michezo hiyo mitatu, nyota huyo wa Simba alifanikiwa kufunga mabao matatu.
Kwa upande wa tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi, Steven Barker aliibuka mshindi baada ya kuwashinda Florent Ibenge wa Azam FC na Juma Mgunda wa Namungo FC.

Barker aliiongoza Simba kushinda michezo yote mitatu iliyocheza ndani ya mwezi Oktoba, matokeo yaliyoiwezesha timu hiyo kupanda kutoka nafasi ya pili hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Wakati huo huo, Kamati ya Tuzo imetangaza washindi wengine katika vipengele mbalimbali. Hassan Mubiru wa Azam FC, Elie Mpanzu wa Simba na Selemani Bwenzi wa Simba wameteuliwa kuwania Tuzo ya Bao Bora la Mwezi Oktoba.
Katika kipengele cha Meneja Bora wa Uwanja, Jackson Mwendwa wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ametwaa tuzo hiyo kwa mwezi Oktoba.
Aidha, Ramadhan Kalanje wa KMC amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba katika Ligi ya Championship ya NBC, akiwashinda Abdulkari Segeja wa Kigamboni na Hamdan Ally wa Transit Camp.
Kwa upande wa makocha wa Championship, Awadh Juma wa Mtibwa Sugar amechaguliwa kuwa Kocha Bora baada ya kuwashinda Habibu Kondo wa Bandari na Mohamed Muya wa KMC.