Mkurugenzi Mkuu wa tathmini, Usajili na Maendeleo klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Walter Steenbok ameeleza kuvutiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na klabu ya Yanga akiamini watafanikiwa katika mipango yao
Jana Steenbok aliwaongoza wenzake kutoka nchi za Afrika Kusini, Latvia na Uganda kuonana na Viongozi, Wafadhili, Wadhamini na Wahisani wa Klabu ya YangaΒ kujadili maswala mbalimbali kuhusu soka la Bara la Afrika na uwekezaji endelevu kwenye vipaji vya soka hususani katika klabu ya Yanga
Wadau hao pia walitembelea Makao Makuu ya klabu ya Yanga na kujionea mambo mbalimbali
Steenbok ameeleza kushangazwa na ukubwa wa Yanga, kwa uwekezaji wanaofanya, wana nafasi ya kuwa kitovu cha soka Tanzania
"Yanga ni timu kubwa sana, nimeona wao ni klabu ya michezo mbalimbali, wana mashabiki wengi. Nimeona miundombinu yao, wana nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha soka hapa Tanzania. Nimevutiwa na duka lao ambalo wanauza jezi na bidhaa nyingine za klabu, nimeshuhudia watu wengi wakifika kununua jezi. Ni chanzo kizuri cha mapato"
"Ni jambo zuri kuwa na mipango, kuweka malengo na kuhakikisha unafikia malengo yako. Jambo muhimu pia wanapaswa kuwa na mfumo mzuri wa kukuza wachezaji kuanzia umri mdogo miaka 9,11 na kuendelea. Huu ndio utaratibu ambao timu kubwa zinafanya," alisema