Kocha wa zamani wa timu za Taifa za Kenya na Guinea ya Ikweta Sebastian Migne, amesema kuwa atakuwa tayari kujiunga na Yanga kama mabingwa hao wa kihistoria watahitaji huduma yake
Mapema wiki hii ziliibuka tetesi kuwa Yanga imemuhitaji kocha huyo ikiachana na mpango wa kumuajiri Hubert Velud ambaye ndiye aliyekuwa akitarajiwa kuchukua mikoba iliyoachwa na Cedric Kaze
Kocha huyo wa timu ya Taifa ya Sudan ilielezwa kuwa angejiunga na Yanga mwezi Julai na hivyo kupelekea mabosi kumrejesha Juma Mwambusi na kumkabidhi jukumu la kukinoa kikosi mpaka mwishoni mwa msimu
Migne amethibitisha kuwa na Mawasiliano na Yanga lakini hakuweka wazi kama kuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa
"Ndio kumekuwa na Mawasiliano, lakini siwezi kukwambia zaidi ya hapo, ni vyema ukawasiliana na viongozi wa Yanga wanaweza kuwa na la kusema. Muhimu subiri.." Migne aliuambia mtandao wa Goal
"Nimependa kufanya kazi Afrika Mashariki, hivyo kama kutakuwa na makubaliano kwa nini nisirudi?"
Migne aliiongoza Harambee Stars kwenye michuano ya Afcon 2019, timu yake ikipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tanzania katika michuano hiyo
Aidha ndiye aliyekuwa kocha wa Guinea ya Ikweta iliyokuja kucheza na Tanzania mchezo wa kuwania tiketi ya fainali za Afcon 2021, mchezo ambao Tanzania ilishinda mabao 2-1
Baada ya mlipuko wa corona, Migne aliachana na Guinea ya Ikweta, sasa yuko tayari kwa majukumu mapya