Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela ameeleza kusikitishwa na kifungo alichopewa na Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akieleza amefungiwa sababu ya kutekeleza majukumu yake
Jana kamati ya Maadili ilitangaza kumfungia Mwakalebela miaka mitano kutojihusisha na shughuli za soka pamoja na kulipa faini ya Tsh Milioni 7 kutokana na makosa ya uchochezi na kutoa taarifa ya uongo
Mwakalebela aliyewahi kuhudumu kama Katibu Mkuu wa TFF, amesema chombo hicho kimeendelea kufanya maamuzi yake kwa upendeleo kwa kuwafungia viongozi wa Yanga kwa makosa mabayo pia yanafanywa na viongozi wengine
"Sisi sio watu wa kwanza kulalamika kufanyiwa hujuma. Simba waliongea, Mo Dewji aliongea, Haji Manara aliongea na hata Barbara aliongea lakini unaona kabisa akiongea Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela ndio linaonekana ni kosa. Ndio maana ninasema kuna siku nitaongea"
"Unapomtuhumu Mwakalebela kwamba ni mchochezi wajue mgongoni kwangu ni watu Milioni 20 ambao ni wapenzi na wanachama wa klabu ya Yanga. Wanayanga wanajua kinachoendelea na itafika siku tutaiambia Serikali na naamini itasema"
"Wanachama, Wapenzi na Mashabiki wa klabu ya Yanga wajue kwamba niliyaongea hayo nikiwa na lengo la kuitetea klabu yao. Nafahamu wanajaribu kututoa katika lengo letu. Lakini niwahakikishie, tumejipanga vizuri, tumeongoza ligi kwa miezi sita mfululizo, hakuna timu iliyowahi kufanya hivyo," alisema Mwakalebela