Baada ya Simba kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita, wametinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa matokeo ambayo kimahesabu yataipa Tanzania nafasi nne katika michuano ya CAF msimu ujao
Timu zitakazomaliza nafasi ya 1 na 2 katika msimamo wa ligi kuu ya Vodacom, zitajihakikishia kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa wakati nafasi ya tatu atashiriki kombe la Shirikisho akiungana na mshindi wa kombe la Azam
Hata hivyo haya sio matokeo ambayo yanapaswa 'kuishughulisha' sana Yanga kwani lengo kuu ni kutwaa ubingwa ambao moja kwa moja utawahakikishia tiketi ya kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao
Kabla ya kukumbana na rungu la TFF jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela alipata kusema Yanga itapigania tiketi yake ya michuano ya ligi ya mabingwa kwa kutwaa ubingwa na sio vinginevyo
"Sisi hatufikirii kubebwa na timu yoyote, timu yetu inapambana kushinda ubingwa kwani tunafahamu tukiwa mabingwa tutapata tiketi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao. Nafasi yetu tutaipigania wenyewe..!," alisema
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama 50 baada ya kushuka dimbani mara 23
Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 46, huku pia wakiwa na mechi tatu za viporo
Yanga inapaswa kuchanga karata zake vyema katika michezo 11 iliyobaki ili kuweza kushinda ubingwa mbele ya watani zao Simba
Miongoni mwa matokeo muhimu ambayo Yanga itahitaji, ni ushindi dhidi ya Simba katika mchezo utakaozikutanisha timu hizo May 08