Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa anatarajiwa kukutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu ya Yanga kumaliza tofauti zilizopo baina ya pande hizo mbili
Hayo yamesemwa na Katibu wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Dk Hassan Abbasi leo kufuatia tetesi za Yanga kutaka kufanya maandamano ya amani kupinga kile wanachoamini uonevu wa TFF dhidi yao
"Nimesikia watu wanataka kuandamana sijui maeneo gani, hawa watu wa Yanga wanaona kwamba kuna matatizo kwenye TFF, hizi kelele zimekuwa nyingi"
"Kwa hiyo kama Serikali huwezi ukakaa kimya ukisikia watu wanataka kuandamana iwe ni kweli au wanatishia"
"Kesho Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo amewaita Yanga kuwasikiliza kuna nini, lakini pia amewaita TFF wenyewe kwa upande mwingine nao kuwasikiliza kwamba kuna nini hiki, Kisha taratibu zile za kawaida za kimfumo wa mpira zitafuatwa"
"Lakini kesho hili ningeomba pia nilisisitize kwamba kama kuna malalamiko yoyote, wadau watulie Serikali ipo, inasikiliza na vyombo vipo, yale yanayopaswa kubaki kwenye kanuni za michezo yatabaki, yanayohitaji mwongozo na maelekezo ya Serikali tutatoa, hivi ndivyo tunavyopaswa kwenda," amesema Dk Abbas