Baada ya klabu ya Yanga kuwasilisha malalamiko yao kwa Serikali wakidai kuonewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Serikali imeziagiza pande zote mbili kukutana ili kupata mwafaka wa changamoto zinazojitokeza baina yao
Kauli ya Serikali ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya michezo Yusuf Singo baada ya kusikiliza malalamiko ya Yanga na pia kusikia upande wa TFF
"Malalamiko ya Yanga yalikuwa mengi, kubwa walidai kutotendewa haki na Shirikisho na waamuzi. Uongozi wote wa Yanga ukiongozwa na Mwenyekiti, Kaimu Katibu Mkuu, Mwanasheria na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walikuja kuzungumza nasi," alisema Singo
"Pia tulifanya kikao na watu wa TFF, tuliwaeleza malalamiko ya Yanga na kikubwa ambacho TFF walituambia ni kuwa wanafanya kazi kwa kufuata taratibu na wana kamati zao ambazo zinafanya kazi kwa weledi, hivyo kama kuna makosa yanatokea huko"
"Tumewaagiza wakae kikao cha pamoja Jumatatu wamalize tofauti zao, kisha watupe mrejesho wa kilichojiri kwenye kikao chao," aliongeza Singo
Baada ya kamati ya Maadili ya TFF kumfungia Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela pamoja na kumtaka alipe faini ya Tsh Milioni saba, Yanga ililazimika kuwasilisha malalamiko yake Serikalini wakipinga kifungo hicho
Taarifa iliyotolewa na Yanga juzi ilibainisha kuwa Mwakalebela alifungiwa kwa kuzungumza masuala ambayo alitumwa na klabu ya Yanga na kuwa hazikuwa kauli zake binafsi
Yanga imelalamika kuwa kumekuwa na mfululizo ya matukio ya kutotendewa haki na Shirikisho hilo la usimamizi wa soka Tanzania