Klabu ya Yanga imemtambulisha rasmi Nasreddine Mohamed Nabi kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua mikoba iliyoachwa na Cedric Kaze aliyefutwa kazi mwezi uliopita
Nabi amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu
Nabi raia wa Tunisia, amekuja na Kocha Msaidizi pamoja na mtaalam wa viungo
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Nabi ameeleza kufarijika kujiunga na Yanga, moja ya klabu kongwe na yenye historia kubwa barani Afrika

Nabi anayezungumza lugha ya kiarabu na kifaransa, amesema ujio wake nchini ni kwa ajili ya kazi maalum ya kuirudisha Yanga katika ubora wake
"Naifahamu Yanga, ni timu yenye historia kubwa hapa Tanzania, ndio timu yenye makombe mengi. Nafahamu kipindi cha karibuni timu imepoteza makali yake hivyo nimekuja kuhakikisha tunairejesha katika ubora wake na kutengeneza timu itakayoshindania makombe Afrika"
"Bila ya kuathiri mipango ya msimu huu, napenda nipate muda niweze kuifanya kazi kwa ufasaha. Nimejiandaa na nina kila kigezo cha kuifanya kazi hii iliyopo mbele yangu."
"Nalifahamu vizuri soka la Afrika kwani nimefanya kazi katika nchi zote zenye ushindani na nimeziongoza timu kufanya vizuri katika ligi za ndani na ligi ya mabingwa barani Afrika"
"Mimi sio kocha wa bla.. bla, mimi ni vitendo tu, sipendi porojo, nataka Yanga iwe timu kubwa," alisema Nabi